Kijana mmoja alisafiri kwa meli na familia yake wakiwa katikati ya safari yao meli ilianza kuzama. Watu wengi pamoja na familia nzima ya yule kijana walikufa maji wakati wanajaribu kujiokoa kwa kuogelea, lakini yule kijana alifanikiwa kushika ubao ulioelea majini akaanza kuelea nao, maji yalimpeleka hadi kisiwa cha mbali sana ambako hakukuwa na watu wala wanyama isipokuwa wadudu tu! Alifika ufukweni amechoka sana na asiyeamini tukio lililotokea, akaishi huko
kwa kula matunda.
Aliweza kujenga ka-kibanda kwa shida sana maana hakuwa na shoka wala panga, hatimaye akaanza maisha mapya. Aliishi muda mrefu kisiwani na tayari alishazoea mazingira yale ya shida japo shida haizoeleki. Mara zote nyakati za jioni aliwasha moto kwa kupekecha vijiti. Siku moja kama kawaida yake aliwasha moto nje karibu na kibanda chake, aliota moto muda mrefu hatimaye akapitiwa na usingizi. Alilala hapo hapo hadi usiku wa manane aliposhtushwa na joto kali lisilo la kawaida.
Kumbe moto ulishika nyasi za kibanda chake na kibanda chote kikaungua moto.Alilia sana na kumlaani sana Mungu kwa mateso hayo akisema "Hivi Mungu nimekukosea nini mpaka unitese hivi? Pamoja na shida zote hizi bado unaniongezea shida nyingine, umeteketeza makazi yangu ilhali nimejenga kwa shida, Hukuridhika kunitenga mbali na familia yangu nilipoishi kwa raha? Hukuridhika kuwaua ndugu zangu wote baharini? Kwanini Mungu umekuwa mkatili hivi?Bora nife tuu maana nimeshachoshwa na hizi shida!" akaendelea kulalamika na kumlaani Mungu hadi kukapambazuka. Ilipofika asubuhi aliiona meli ikija kwa mbali kuelekea alipo, alishangaa maanahakuna meli yoyote inayoweza kwenda kisiwa kile labda kama imepotea njia.
Meli ilipofika ufukweni yule kijana akaifuata, alienda moja kwa moja hadi kwa kapteni.Kapteni akamwambia "tuliona moto mkali sana usiku tukahisi ni meli inawaka moto tukasema tuje ili tutoe msaada..kwa kweli tumetembea masaa mengi sana hadi kufika hapa, mshukuru Mungu maana ametumia moto kutuleta hapa" yule kijana kusikia hivyo alilia sana, akajilaumu kwa jinsi alivyo mnung'unikia Mungu. Akaelewa kuwa Mungu ana njia nyingi za kuleta msaada kwa mtu. Akapiga magoti akatubu huku akimshukuru Mungu. Safari ya kurudi nyumbani ikaanza.
FUNDISHO: Mwenyezi Mungu ni mwema daima na mwenye hekima isiyo na mfano.Wakati mwingine mambo magumu tunayopitia yanakuwa chini ya hekima zilizotukuka za mwenyezi Mungu bila ya sisi kutambua. (📖 Hashim Seki)