Baadhi ya watu ambao husafiri kwenye Meli au chombo chochote cha majini ( boti n.k ) hujisikia vibaya na kutapika wanapokuwa kwenye vyombo hivyo .
Je unafahamu chanzo cha hali hiyo inayowakumba baadhi ya watu ?
Chanzo cha hali hiyo ni Ubongo wa binadamu kushindwa kutafsiri taarifa vizuri, Moja ya kazi ya Ubongo wa binadamu ni kutafsiri na kutambua mwendo au mjongeo ( movement) wa mwili kwa kutumia sehemu kuu tatu ambazo ni Macho , Masikio ( hususani sehemu ya sikio ya ndani ) na Misuli pamoja na viungo ( joints ).Kazi ya ubongo ni kuchukua taarifa kutoka sehemu hizo za mwili na kutafsiri mjongeo na mkao wa mwili
Unapokuwa ndani ya chombo cha majini Macho hupeleka taarifa kuwa mwili hautembei kwa kuwa ukiwa ndani ya chombo cha majini unaona kama hakitembei na pia Misuli na viungo hupeleka taarifa kuwa mwili haujongei na umetulia lakini Masikio huweza kuhisi mawimbi ya maji na mwendo wote wa chombo hicho na kupeleka taarifa kuwa chombo kinatembea.
Ubongo hushindwa kutafsiri taarifa hizo zinazotofautiana ( zinazokinzana ) kutoka sehemu hizo za mwili na kupelekea Mtu kujisikia vibaya na hata kichefuchefu , tumbo kuuma , kukosa hamu ya kula au kutapika .
Hali hii pia huwatokea baadhi ya watu ambao wanasafiri nchi kavu ( barabarani ) kwa umbali mrefu .
Hali hii ni ya kawaida ndani ya mwili wa binadamu na sio ugonjwa ( 🖊 Luqman Kisokora )