KISA CHA KUSISIMUA
Siku moja jioni katika mji fulani, kulikuwa na basi likisafiri kutoka mji huo kuelekea mji mwingine. Lilikuwa ni basi kubwa na limejaa abiria. Wakati wakiendelea na safari, ghafla mvua kubwa iliyoambatana na radi ikaanza kunyesha. Dereva hakuogopa, wala abiria, wakaendelea na safari. Mara wakati wanaenda, radi ikaanza kufuatilia gari. Kila wakienda, radi inapiga karibu na basi kana kwamba inalifuata basi.
Basi likisimama, radi inapiga pembezoni mwa basi. Dereva kuona hivyo, akasimamisha gari mita 5 kutoka kwenye mti, akawaambia abiria, "Humu ndani ya basi, kuna mtu ambaye leo ni siku yake ya kufa, tena kufa kwa radi. Ili tusife wote, nataka kila abiria ashuke akaguse mti ili anayepigwa na radi, apigwe wengine wasife kwa ajili yake. " Abiria wakitetemeka, wakaanza kushuka mmoja mmoja. Unaenda unagusa mti , kisha unarudi kwenye basi. Abiria wote pamoja na dereva mmoja mmoja, wakaenda, wakagusa mti na kurudi bila dhara lolote! akawa kabaki abiria mmoja tu, ambaye alikuwa hajagusa mti.
Abiria wote kwa macho ya hasira wakamwambia akaguse mti. Akawa anaogopa kufa. Akagoma. Wakamlazimisha kwa nguvu sana na kumtoa nje. Yule abiria akiwa amefumba macho, akaenda akagusa mti. Hamadi bin Vuu! Radi kali sana ikalipiga basi, abiria na wote waliokuwemo, wakafa palepale. Kumbe uwepo wake ndio ulikuwa unazuia abiria wengine wasidhurike na radi.
MAFUNZO
1. Unapofanikiwa, huwezi jua uwepo wa nani umefanikisha mafanikio yako, usichukue sifa zote peke yako. Wapatie na wengine bila kumsahau MUNGU.
2. Unaweza kujiona huna thamani sehemu ulipo, iwe darasani, kazini,barabarani au hata kwenye familia bila kujua kama uwepo wako ni wa muhimu sana kwa ustawi wa wengine.
3. Usimtenge wala kumnyanyasa mtu au jirani yako, huwezi jua uwepo wake ni kwa ajili gani.
(📖 Hashim Seki)