Katika jamii zetu za kiafrika kumekuwa na migogoro mingi ndani ya ndoa , moja ya migogoro hiyo ni kupata mtoto wa jinsia fulani ( kike au kiume ). Kumekuwa na misemo kama vile " Yule mwanamke anazaa watoto wa kike pekee " , Mara utasikia " Huyu wifi hafai yeye analeta watoto wa kike tuu " .
Je kauli hii ina ukweli kiasi gani kisayansi na ni haki kumlaumu mwanamke kuhusu kuzaa watoto wa jinsia fulani pekee ?
Tukienda kisayansi Mtoto hupatikana kutokana na muunganiko wa yai la kike na mbegu ya kiume( sperm ) . Kwenye muunganiko huo Mama hutoa kromosomu ( XX ) na Baba hutoa Kromosomu ( XY ) na pia ikumbukwe kuwa kila mwanadamu anamebeba Kromosomu 2 yaani XY kama ni Mwanaume na XX kama ni mwanamke .
Mwanamume hutoa mamilioni ya mbegu na Mwanamke hutoa yai moja tuu. Hivyo kati ya Mamilioni ya mbegu yanayotolewa na Mwanamume , mbegu ( sperm) moja tuu ndiyo ambayo itaungana na yai la mwanamke.
Hivyo kwenye muunganiko wa mbegu hizo ni Baba ndiye anayepelekea mtoto kuwa wa jinsia gani kwa sababu anatoa X na Y , wakati Mama anatoa X na X tuu .
Hivyo endapo Mbegu yenye Kromosomu X ya Baba itaungana na Yai la mama lenye Kromosomu X, basi Mtoto atakuwa wa Kike XX ( X ya Baba na X ya Mama ).
Na kama Mbegu yenye Kromosomu Y ya Baba itaungana na Yai la mama lenye Kromosomu X, Mtoto atakuwa wa Kiume XY ( Y ya Baba na X ya Mama ) .
Hivyo kisayansi na kiuhalisia tunafanya makosa pale ambapo jamii inawalaumu wanawake kuhusu kupata watoto wa jinsia fulani . Hivyo Sio vizuri kumlaumu mtu yeyote kuhusu jinsia ya mtoto
NB : WATOTO WOTE NI SAWA NA WANAHITAJI MALEZI NA UPENDO KUTOKA KWA WAZAZI WOTE WAWILI