Kuku Kwenye Historia Ya NEW BALANCE

Unapozungumzia swala la kupendeza ( kuwaka ) mojawapo ya sehemu muhimu sana ni kiatu ( watoto wa mjini wanaita "Mguu" ) . Kiatu kinachukua sehemu kubwa mno ya muonekano wako . Kampuni za viatu zipo nyingi mno ila unapozungumzia kampuni zenye soko kubwa na zinazopendwa sana duniani huwezi kuiacha NEW BALANCE . Hii ni moja ya kampuni kongwe ya kuzalisha na kusambaza viatu,nguo na bidhaa nyingine za mavazi duniani . Ukitaka kuijiua kwa haraka , wananembo ya herufi kubwa ya N pembeni mwa viatu vyao ( sasa nadhani utakuwa ushapata picha kamili ya kampuni hiyo , huwezi kupita sehemu zenye watu wengi mfano kariakoo bila ya kuona mtu katupia new balance ) .

Kampuni hii ina zaidi ya miaka 117 kwa sasa ( yaani karne moja ) ambapo ilianzishwa rasmi mwaka 1906 .
Ukikaa na wasawahili watakwambia mbuyu ulianza kama mchicha , yaani kila kitu kikubwa unachokiona kukianzia hatua ya chini kabisa . Hii ni kweli hata kwenye kampuni ya NEW BALANCE , kwani hata yenyewe haikuanza kuzalisha viatu moja kwa moja , je unajua walianza kuzalisha bidhaa gani ? 

Mnamo mwaka 1906 bwana WILLIAM J RILEY( mhamiajj kutoka Ireland ) alianzisha kampuni ya kuzalisha visaidizi unyayo ( soli ) [ arch support ] ili kusaidia kupunguza maumivu kwa watu wanaovaa viatu kwa muda mrefu . Na hivyo visaidizi vya unyavyo ndiyo vilivyoleta jina la NEW BALANCE ( yaani balance mpya ) .


Soli hizo zilikuwa na pembe 3 zilizokuwa zikisaidia  kushikilia vizuri unyayo pale zinavyovaliwa .
Inaelezwa kuwa Bwana RILEY alipata wazo la kutengeza soli hizo ili kusaidia watu wanaopata maumivu ya miguu pindi wanapovaa viatu , na wazo la kutengeneza soli yenye pembe 3 zinazoshikilia ( 3 supports )  ni kutokana na kuangalia miguu ya kuku wake na kuona kuwa wanasimama  bila ya shida yeyote huku miguu yao ikiwa na vidole vitatu vya chini  vinavyoupa mguu balance  . Baada ya kuangalia kuku wake kwa makini na hapo ndipo mwanzo wa kutengeneza soli hizo ilipoanza , kwa kuwa ilikuwa ni soli mpya na yenye muundo tofauti na hapo ndipo akaamua kuita NEW BALANCE ( Balance mpya ) .



Na kampuni hiyo iliitwa NEW BALANCE ARCH SUPPORT COMPANY ambapo ilikuwa huko Boston Marekani. 
Mnamo mwaka 1927 RILEY alimuajiri bwana AUTHUR HALL kuwa mtu wake wa mauzo , ambapo HALL alikuwa ananunua soli kwa $3 kutoka kwa RILEY na yeye anauza kwa $5 . Na hatimaye mwaka 1934 kipindi cha Anguko kubwa la uchumi ( GREAT ECONOMIC DEPRESSION ) RILEY akamtaka HALL akawa partner wake kwenye biashara ili kuweza kuvuka kwenye kipindi hicho kugumu .
Mnamo mwaka 1938 Ulikuwa ni mwaka wa kihistoria kwa kampuni hiyo changa ambapo walitoka kwenye kutengeneza soli za viatu na kuhamia kwenye kutengeneza kiatu Chao cha kwanza cha riadha ambacho kilibuniwa na Bwana RILEY , kiatu hicho kilikuwa ni kwa ajili ya wakimbiaji wa klabu ya riadha iitwayo BOSTON BROWN BAG HARRIERS .
Baada ya Manifikio hayo kampuni ikazidi kujipanua na ilipofika mwaka 1941 wakaanza kuzalisha viatu vya michezo mbalimbali kama vile Tennis , Boxer na Baseball .

Baada ya takribani miaka 44 ya kuendesha kampuni hiyo , Mnamo mwaka 1950 RILEY alistaafu kazi na kumuacha partner wake HALL kuongoza kampuni hiyo , Waswahili wanasema kila chenye mwanzo kina mwisho kwani baada ya miaka mitatu ya kuachiwa kampuni yaani 1953 naye bwana HALL aliamua kustaafu na kuiuza kampuni hiyo kwa USD 10,000 kwa Binti yake ( ELEANOR ) na Mkwe wake ( PAUL KIDD ) na zama mpya za kampuni ya NEW BALANCE zikaanza kutokana na kuingia kwa mawazo mapya kutoka kwa damu changa .

Hatimaye mnamo mwaka 1960 PAUL na mkewe wakazalisha kiatu kiitwacho TRACKSTER maalumu kwa wanariadha . Kiatu hicho kulizalishwa Kwenye basement ya nyumba hiyo . Na mbinu iliyotumika kukipromote kiatu hicho ni kupitia kutangaza kwa watu wao wa karibu kwa njia ya ana kwa ana , kiatu hicho kilitokea kupendwa mno na kulikuwa na size tofauti kwa watu mbalimbali kulingana na muundo wa miguu ya watu , kiatu hicho kikazidi kupata umaarufu .


Mwaka 1961 wakaendelea kukipromote kwa kukiuza kwa makocha na sehemu za maonesho ya biashara . Timu za riadha za vyuo kama MIT na TUFFS walikuwa wanatumia viatu hivyo kutoka kampuni ya NEW BALANCE viitwavyo TRACKSTER. 
Wahenga wanasema mgaa gaa na upwa hali wali mkavu , na hatimaye juhudi za mtu na mke wake zilizaa matunda pale ambapo kiatu hicho kilivaliwa kwa mara ya kwanza kwenye Marathon ya mwaka 1961 na KENNETH COOPER MD.
Tukio hilo lilifungua zaidi milango ya umaarufu wa kiatu hicho na kampuni hiyo kwa kiasi kikubwa mno .

Mnamo mwaka 19 . 04 . 1972 Siku ya Marathon huko Boston . Kijana wa miaka 28 JIM DAVIS alinunua kampuni hiyo kutoka kwa ELENOR na Mume wake baada ya kuiongoza kwa mafanikio ya takribani miaka 19 . JIM DAVIS akiwa kama mmiliki mpya wa NEW BALANCE alikuwa na wafanyakazi 6 tuu ambao walikuwa kwa siku wanatengeneza pair 30 za viatu ambapo mauzo kwa mwaka yalikuwa hayafiki hata USD 1M . Na viatu hivyo vilikuwa vinapatikana huko Boston tuu dunia nzima .

NEW BALANCE KUINGIA DUNIANI .
Mwaka 1976 unakuwa ni mwaka wa mageuzi kwa kampuni ya NEW BALANCE kwa sababu matukio makubwa yakiyotokea yalikuwa ni .
1. Kwa Mara ya Kwanza Viatu vya NEW BALANCE viliwekwa ile herufi N .
2 . Soko la Ulaya lilikuwa kwa kiasi kikubwa na duniani kwa ujumla .
NEW BALANCE 302 kilikuwa kiatu namba moja duniani kwa orodha iliyotolewa na RUNNING WORLD .

Huo ukawa ni mwanzo wa NEW BALANCE kutambulika duniani kwa ujumla na hadithi ikiwa nyingine mpaka sasa .
Kwa mwaka 2022 Kampuni hiyo ina zaidi ya wafanyakazi 8,000 na inafanya biashara kwenye zaidi ya nchi 120 duniani kote ikiwa na Mapato ( Revenue ) makubwa takribani Shilingi za kitanzania Trilioni 10.29 ( USD 4.4B )

Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form